Thursday, 22 June 2017



Shirika la Kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limeonya kwamba watoto takriban milioni tano nchini Iraq wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.
Shirika hilo limesema watoto wa nchi hiyo hususan wale wote walio katika mji wa Mosul, ambako majeshi ya Iraq yanapambana vikali na wapiganaji wa Islamic state, wamejikuta katika ghasia na umasikini usio na mwisho.
Takwimu zilizooneshwa na UNICEF zinaonesha kuwa nusu ya wagonjwa wanaotibiwa katika vituo vya watu wenye maradhi ya wasiwasi na kuchanganyikiwa kutokana na hofu, (magonjwa mabaya ya akili) magharibi mwa Mosul ni watoto.
Kwa mujibu wa ripoti, watoto wapatao laki nane nchini Iraq kote, wamepoteza mzazi japo mmoja.
Mashirika ya misaada yanasema fedha zaidi zinahitajika haraka kuweza kusaidia kuwalinda watoto wa Iraq, kutokana na mapigano hayo.

Saturday, 11 March 2017

Chirwa, Msuva kupeleka maumivu Zanaco leo


KOCHA wa Yanga, George Lwandamina, amesema hakuna kitakacho wazuia leo kupata ushindi kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa Afrika huku akiamini washambuliaji wake, Simon Msuva na Obbrey Chirwa watapeleka kilio kwa wapinzani wao Zanaco.

Yanga inacheza na Zanaco leo kwenye Uwanja wa Taifa kuanzia saa 10:00 jioni ukiwa ni mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Msuva na Chirwa wamekuwa kwenye kiwango cha juu huku wakiisaidia Yanga kupata ushindi kwenye michezo yao.

Wiki iliyopita Chirwa alionyesha kiwango cha juu kwenye mchezo wa kombe la FA dhidi ya Kiluvya United na kufunga magoli manne katika ushindi wa bao 6-1 waliupata Yanga.

Msuva, anayeongoza kwenye orodha ya wafungaji kwenye ligi kuu msimu huu akiwa na magoli 12, amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Yanga na leo anatagemewa kupeleka kilio kwa Wazambia hao.

Akizungumza na gazeti hili jana, Lwandamina, alisema kuwa hana hofu na mchezo wa leo kwa kuwa kila kitu amekiweka sawa na kazi imebaki kwa wachezaji wake tu.

"Naamini kwa kile tulichokifanya mazoezini na kama wachezaji watafuata maelekezo yangu, nina uhakika wa ushindi mzuri kesho (leo)," alisema Lwandamina.

Alisema kuwa anawafahamu wapinzani wao wa leo kwa kuwa amekutana nao mara kwa mara kwenye Ligi ya Zambia wakati alipokuwa akiifundisha Zesco ya nchini humo.

Lwandamina, alisema watacheza soka la kushambulia muda wote na kujaribu kuwabana wapinzani wao wasitengeneze nafasi ya kupata bao litakalovuruga mipango yao.

Mchezo wa leo utachezeshwa na mwamuzi Aden Abdi kutoka Djibout akisaidiwa na Hassan Yacin na Farhan Salime.

Wakati Yanga wakicheza leo Uwanja wa Taifa, wawakilishi wengine wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam FC watashuka Uwanja kesho kuumana na Mbabane Swallows kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Mchezo huo wa hatua ya kwanza umepangwa kuanza saa 1:15 usiku.Chirwa, Msuva kupeleka maumivu Zanaco leoChirwa, Msuva kupeleka maumivu Zanaco leo


Simba uwanjani Dodoma leo

KATIKA kujiimarisha kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, vinara wa ligi hiyo, Simba leo watashuka kuwakabili Polisi Dodoma katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani humo.

Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, aliomba mechi hiyo ya kirafiki ili kuwafanya wachezaji wake waendelee kuwa na 'joto' la mashindano wakati michezo ya Ligi Kuu Bara imesimama kwa muda.

Omog alisema kuwa kwake mechi ya leo anaipa uzito kwa sababu anataka kuona wachezaji wake wanashinda na kuwafurahisha pia mashabiki wa timu hiyo wa mkoa huo.

"Ni mechi ya kirafiki, lakini kiufundi tunaiangalia kwa jicho lile lile linalofanana na pale tunapocheza na Yanga, hatutaki kupoteza mechi yoyote kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu huu," alisema Omog.

Kocha huyo wa zamani wa Azam FC aliongeza kuwa licha ya kuwa na majeruhi, amewataka wachezaji watakaopata nafasi ya kucheza kuonyesha uwezo wao na kuwania namba katika kikosi cha kwanza.

"Hii ni timu, mchezaji atakayecheza vizuri atanishawishi kumpanga katika kikosi cha kwanza au kusubiri kwenye orodha ya wachezaji 18, kuna baadhi ni wazuri wakianza au wakiingia baada ya kuwasoma wapinzani," Omog aliongeza.

Baada ya mechi ya leo, Simba inatarajiwa kuelekea Tabora kucheza mechi nyingine ya kirafiki huku Jumapili ikitua Arusha kuwakabili wenyeji Madini FC katika mchezo wa hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la FA.

Mimba zakatisha masomo wasichana 48


WASICHANA 48 katika shule za msingi na sekondari wilayani Karagwe mkoani Kagera, wameacha shule kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo mimba.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, Adeodata Peter, alisema wanafunzi 25 walipata mimba, wanne waliolewa na tisa walitoroshwa na kuacha masomo kwa mwaka 2016.

Adeodata alibainisha kwamba halmashauri hiyo imewachukulia hatua mbalimbali za kusheria wanaume wote waliohusika kuwapa mimba wanafunzi hao.

Kwa mujibu wa Adeodata, miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kufungua mashtaka na mpaka sasa baadhi yao wameshtakiwa na kuhukumimwa.

Hata hivyo, Adeodata hakufanya zaidi kuhusu adhabu za zilizotolewa na mahakama ukiwamo muda wa vifungo.

Hata hivyo, aliongeza kuwa zipo hatua kadhaa zinazoendelea kuchukuliwa katika halmashauri za kukabiliana na matukio hayo.

Miongoni hatua hizo, Adeodata alisema kuwa ni Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe inaimarisha idara ya jinsia na watoto na kuwezesha wasichana kutekeleza majukumu yao kwa jamii.www.omblox.blogspot.com

Viroba vya mil. 130/- vyakamatwa


MSAKO wa kukamata pombe kali aina za viroba mkoani Dodoma umeshika kasi, baada ya Jeshi la Polisi kukamata shehena yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 134.9.

Polisi walikamata shehena hiyo ya viroba kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA) na Mamlaka ya Mapato Tanzani (TRA).

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Lazaro Mambosasa, alisema walikamata katoni 2,199 katika wilaya za Dodoma na Mpwapwa zenye thamani ya Sh. 134,954,500.

“Huo ni mwendelezo wa oparesheni ya kutekeleza agizo la Serikali la kukamata wauzaji, wasambazaji, na watumiaji wa pombe iliopo katika vifungashio vya plastiki maarufu kwa jina la viroba ambayo imepigwa marufuku tokea Machi Mosi mwaka huu,” alisema Mambosasa.

Aliwataja waliokamatwa na bidhaa hiyo kuwa ni mkazi wa Area C, Consolata Mallya (58) kutoka kampuni ya Cowike Enterprises LTD, ambaye alikutwa na viroba Original na katoni 421, na Zed 1248.

Wengine ni mkazi wa Mpwapwa, Jobu Timoth, ambaye alikutwa na viroba katoni 62.5 na Siloya Mbonyi, wa kampuni ya Takawedo ambaye alikutwa na katoni 444.

Aliwataka wafanya biashara wa dawa za kulevya kuacha mara moja biashara hiyo kwa sababu sio halali.Viroba vya mil. 130/- vyakamatwa

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salam, limetangaza vita dhidi ya matapeli mitandaoni ambao wamekuwa wakitumia jina la mke wa rais mstaafu Salma Kikwete na Mwenyekiti wa IPP, Dk. Reginald Mengi, na kujipatia mamilioni ya fedha kutoka kwa wananchi.

KAMISHNA SIMON SIRRO.
Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna Simon Sirro, alisema matapeli hao wamekuwa wakitumia jina la Salma Kikwete, Dk. Mengi na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, kuwatapeli wananchi.

Alisema wamekuwa wakiwahadaa wananchi watume Sh. milioni moja ili wakopeshwe Sh. milioni 10 na bajaji moja mpya.

Sirro alisema baadhi ya matapeli hao ambao wameshakamatwa, wamekuwa wakifanya utapeli huo kupitia taasisi feki ya ‘Focus Vicoba’ iliyopo kwenye mtandao wa Facebook.

“Kuna uwapo wa taasisi feki ya fedha yenye jina la Focus Vicoba kwenye mtandao wa Facebook na tovuti inayojulikana kwa jina la www.vicobaloanstz.wapka-mob ambayo hutumia majina ya viongozi serikalini na watu maarufu kutapeli,” alisema.

Alisema majina ya viongozi hao yamekuwa yakitumika kufungua akaunti za Facebook na tovuti mbalimbali ambazo matapeli hao hutumia kuwarubuni watu kwamba wanaweza kupata mikopo yenye masharti nafuu na haraka kwa njia ya mtandao.

“Katika ufuatiliaji wa suala hili kitengo cha upelelezi wa makosa ya mtandao cha polisi Kanda Maalumu, kimebaini katika tovuti hiyo picha na jina la Mama Salma limetumika na kwenye ukurasa wa Facebook linatumika jina la Dk. Mengi.

“Wanatumia majina pamoja na namba za simu 0757 308 381 na 0768 199 359 ambazo sio namba za Mama Salma wala Dk. Mengi,” alisema.

Kamanda Sirro alisema ufuatiliaji uliofanyika Desemba 16, mwaka jana uliwezesha kumkamata mtu mmoja (jina tunalo) ambaye kwa sasa ana kesi mahakamani.

Sirro alitoa onyo kwa wale wanaoendelea kufanya udanganyifu na kujipatia fedha kwa njia isiyo halali kupitia mitandao ya kijamii, waache mara moja.

Lema achokoza mapya Arusha


Lema achokoza mapya Arusha
MBUNGE wa Arusha Mjini Godbelss Lema, amechokoza mapya jijini Arusha, kwa kuwapandisha jukwaani wanaye wawili na kudai kama kushtakiwa kwa amri ya polisi iliyomtaka awe mzungumzaji pekee katika mkutano wa hadhara, basi waunganishwe wote na kushakiwa.

Lema alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika shule ya Msingi Ngerenaro kwa ajili ya kusalimiana na wananchi pamoja na wapigakura wake, baada ya kuachiwa na mahakama kwa dhamana wiki iliyopita.

Katika barua ya polisi ya kumruhusu kufanya mkutano jana, walimtaka kuwa mzungumzaji pekee katika mkutano huo, lakini Lema akasema amewapandisha jukwaani watoto hao ili kama kumshtaki basi waunganishwe wote.

Baada ya kupandishwa jukwaani, Lema aliwaita watoto wake (Briliant na Terence) ambao waliwasalimia wananchi kwa nyakati tofauti kwa salamu za Chadema wakianza kwa kuzungusha ngumi na kutamka People’s.

Wakati wakisalimia wananchi, watoto hao kila mmoja kwa wakati wake waliimba wimbo wa ‘CCM kwisha, kwisha kabisa. Mbende mbende, nyang’a nyang’a…kifo cha mende, chalii; hakuna kulala mpaka kieleweke,’ na kuwafanya mamia ya watu waliokuja kusikiliza mkutano huo kuangua kicheko

Sunday, 26 February 2017

WATU 22 MBARONI RUKWA DAWA ZA KULEVYA


Image result for Dawa za kulevya



WATU 22 wamekamatwa mkoani Rukwa wakituhumiwa kulima, kuuza na kusafirisha dawa za kulevya ikiwemo heroin kufuatia msako maalumu kwa lengo la kukabiliana na uhalifu huo.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi mkoani Rukwa, msako huo ambao umefanyika hivi karibuni katika wilaya zote na kusimamiwa na kamati za ulinzi na usalama, mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari 19 yameteketezwa kwa moto na bangi yenye uzito wa kilo 15 na misokoto 105 ya bangi imekamatwa ambapo heroin iliyokuwa ikisafirishwa kutoka jijini Mbeya kwenye mjini Sumbawanga imekamatwa.
Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi mkoani Rukwa, Mtatiro Nyamhanga ametangaza rasmi vita dhidi ya dawa za kulevya mkoani humo huku wakazi wa kijiji cha Msila ambacho ni maarufu kwa kilimo cha bangi wakiungana na Mwenyekiti wao kulishukuru Jeshi la Polisi kwa msako huo huku wakiwasihi wanaojihusisha na kilimo hicho haramu kuacha mara moja.
Amesema mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanafanyika katika wilaya zote Nkasi, Kalambo na Sumbawanga zenye jumla ya halmashauri nne mkoani Rukwa.
Wilayani Kalambo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Julieth Binyura amethibitishwa kukamatwa kwa watu watano wakituhumiwa kulima bangi kwenye mashamba ya ukubwa wa ekari saba katika kijiji cha Ngoma, Kata ya Katete inayopakana na nchi jirani ya Zambia.
Binyura amewaagiza maofisa watendaji wa vijiji na kata zilizopo wilayani humo kuwabaini wanaolima bangi na kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua za haraka zichukuliwe huku akionya kuwa wakishindwa kufanya hivyo, kila mtumishi wa umma aliyeko katika maeneo hayo ya utawala wasaidie kuwafichua wahalifu hao.
Wilayani Nkasi watu wawili wakazi wa kijiji cha Nkundi kilichopo katika Kata ya Kipande wilayani humo wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma ya kulima bangi.
Waliokamatwa wametajwa kuwa ni pamoja na Oscar Msangawale na Thobias Malambo waliokutwa wanalima bangi kwenye mashamba yao na bustani zao kwa pamoja yakiwa na ukubwa wa ekari moja.
Katibu Tawala wa Wilaya Nkasi , Festo Chonya alidai kuwa walipata taarifa za kuwapo kwa shamba la bangi katika kijiji hicho ambapo Kamati ya Ulinzi na Usalama ilifika eneo la tukio na kukuta bangi ikiwa imelimwa katika shamba lenye ukubwa wa zaidi ya ekari moja.
Akifafanua, alisema shamba la bangi lenye ukubwa wa zaidi ya ekari moja linamilikiwa na Msangawale ambapo Malambo yeye alikutwa na bangi ikiwa imeoteshwa kwenye bustani ya maua iliyopo pembeni ya nyumba yake ya kuishi. Kufuatia msako huo, Polisi walifanikiwa kuiteketeza kwa moto bangi yote iliyovunwa katika shamba hilo

MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA

KATIKA kupambana na uhalifu wa dawa za kulevya, Shirika la Posta Tanzania (TPC), linasimika mfumo wa kisasa utakaogharimu Sh. Milioni 200 wa kudhibiti usalama na kurahisisha utambuzi wa vitu na matukio hatarishi na haramu yanayopitishwa au kujitokeza kupitia mtandao wa shirika hilo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo, Dk Haruni Kondo amesema leo alipokuwa akizungumza jijini Dar es Salaam. Dk Kondo alisema mfumo huo unajumuisha ufungaji wa kamera za kiusalama (CCTV), katika Posta Kuu ya Dar es Salaam, na tayari mzabuni aliyeusimika ameshakamilisha kazi yake na ataukabidhi kwa shirika wiki ijayo. Utazinduliwa rasmi wakati wowote kuanzia hapo.
"Aidha tumesimika mifumo ya kisasa ya kiusalama ikiwa ni pamoja na mashine za ukaguzi wa mizigo katika ofisi zenye uwezekano wa kuwa uchochoro wa uhalifu wa aina hii ikiwa ni pamoja na ofisi za Zanzibar, Kigoma, Dar es Salaam na Arusha," amesema.
Amesema hatua hizo zimechukuliwa na shirika ili kuhakikisha linashiriki na kuchangia kikamilifu jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kupambana na uhalifu, ikiwa ni pamoja na usafirishaji, uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya, usafirishaji na utakatishaji wa fedha haramu, ugaidi, udaganyifu katika utambulisho pamoja na uhalifu mwingine wa kimtandao wa kitaifa na kimataifa.
Mwenyekiti huyo alisema Bodi ya Wakurugenzi ya shirika imedhamiria kuongeza msukumo wa kasi ya usimamizi ili kupambana na uhalifu huo ambao una madhara makubwa kwa jamii.
Amesema hatua hiyo imechukuliwa kwa kuzingatia kuwa matukio ya uhalifu uliopangwa yamekuwa ni changamoto kubwa kwa mashirika ya Posta duniani.
Ametaja vitu visivyoruhusiwa kusafirishwa katika mtandao wa Posta kwa mujibu wa sheria kuwa ni pamoja na dawa za kulevya, bidhaa za kemikali zenye sumu, silaha za moto na milipuko, wanyama hai, nyara za serikali, vifaa vya mionzi, vyakula vinavyooza, betri za aina mbalimbali, vimiminika, fedha haramu, utakatishaji wa fedha na vitu vyovyote hatarishi.


Shirika hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usimamizi wa sheria, kwa hivi sasa limeimarisha uhakiki wa mifumo yake na pia ukaguzi wa barua, vifurushi, vipeto na mizigo ili kujiridhisha juu ya usalama na uzingatiaji wa sheria.

ZIARA YA RAIS WA UGANDA YOWERI MUSEVENI

RAIS John Magufuli ameitaka Kampuni ya Total inayowekeza katika ujenzi wa bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 1,443 kutoka Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga, kuacha visingizio na kuanza ujenzi wa bomba hilo mara moja.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati wa ziara ya siku mbili ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais Magufuli alisema serikali imeshughulikia masharti yote saba ambayo mwekezaji hayo aliyataka.
“Masharti aliyoyataka kwa upande wa Tanzania yameshashughulikiwa yote ikiwa ni pamoja na suala la msamaha wa kodi ya thamani. Hivyo hili si tatizo tena, mhusika aambiwe asitafute visingizio vidogovigo vya kushindwa kujenga halafu akasingizia mahali fulani hawafanyi kumbe yeye ni tatizo.
Alisema pia serikali imetoa fursa nyingi kwa mwekezaji huyo ili kurahisisha kazi yake ya ujenzi wa bomba hilo huku akisisitiza kama kuna mambo madogo madogo yanajitokeza yashughilikiwe huku ujenzi ukiendelea.
Rais Magufuli alisema katika kuonesha dhamira ya kweli ya kuhakikisha mradi huo unafanikiwa, Serikali imeshaanza upanuzi wa bandari ya Tanga ili kuwezesha shughuli za ujenzi wa bomba hilo kwenda vizuri.
“Tanzania tuna uzoefu na masuala ya ujenzi wa mabomba, hili litakuwa bomba la tatu kujengwa kwani kuna bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Zambia (TAZAMA) na lile la la gesi asili (kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam),” alisema.
Aliongeza; “Tumeamua tuwakubalie ndugu zetu waganda, kwa sababau waganda ni ndugu zetu, masuala mazuri ya Uganda ni lazima tuyapokee sisi kwa mikono miwili na ndio maana nimemhahakikishia rais kuwa bomba lilitakiwa lianze kujengwa jana kwa sababu sisi hatuna tatizo.”
Rais Magufuli alisema hata maeneo ambayo bomba hilo litapita ambayo ni ya hifadhi ya barabara, Serikali itahakikisha inalitatua hilo ili kuhakikisha bomba hilo linapita na kujengwa.
Rais Museveni baada ya kufanya mazungumzo na Rais Magufuli kuhusu suala la ujenzi wa bomba la mafuta, aliahidi kufuatilia baadhi ya mambo kwa upande wa nchi yake ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kama ulivyopangwa.
“Tumegundua mafuta mwaka 2006 hata kabla ya Ghana, lakini kwa muda mrefu yamebaki ardhini kwa sababu kuna baadhi ya makampuni makubwa yalitaka kufanya udanganyifu wa njia ya kipitisha mafuta.
“Hatimaye sasa tumepata njia ya kupitisha mafuta, hivyo hatuna sababu ya kuendelea kupoteza muda kwa sababu utatupa fedha ambazo zitasaidia kuboresha miundombinu na kuibadili kabisa nchi yetu,” alisema.
Aidha, viongozi hao wawili wamekubaliana mwekezaji huyo kuanza mchakato wa kuhakikisha jiwe la msingi la ujenzi wa bomba hilo haraka iwekezenavyo.


Rais Museveni ameishukuru serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi miwili ya umeme ambayo itasaidia vijiji vilivyoko Tanzania na vile vya Uganda kupata umeme wa uhakika.