Sunday, 26 February 2017

WATU 22 MBARONI RUKWA DAWA ZA KULEVYA


Image result for Dawa za kulevya



WATU 22 wamekamatwa mkoani Rukwa wakituhumiwa kulima, kuuza na kusafirisha dawa za kulevya ikiwemo heroin kufuatia msako maalumu kwa lengo la kukabiliana na uhalifu huo.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi mkoani Rukwa, msako huo ambao umefanyika hivi karibuni katika wilaya zote na kusimamiwa na kamati za ulinzi na usalama, mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari 19 yameteketezwa kwa moto na bangi yenye uzito wa kilo 15 na misokoto 105 ya bangi imekamatwa ambapo heroin iliyokuwa ikisafirishwa kutoka jijini Mbeya kwenye mjini Sumbawanga imekamatwa.
Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi mkoani Rukwa, Mtatiro Nyamhanga ametangaza rasmi vita dhidi ya dawa za kulevya mkoani humo huku wakazi wa kijiji cha Msila ambacho ni maarufu kwa kilimo cha bangi wakiungana na Mwenyekiti wao kulishukuru Jeshi la Polisi kwa msako huo huku wakiwasihi wanaojihusisha na kilimo hicho haramu kuacha mara moja.
Amesema mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanafanyika katika wilaya zote Nkasi, Kalambo na Sumbawanga zenye jumla ya halmashauri nne mkoani Rukwa.
Wilayani Kalambo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Julieth Binyura amethibitishwa kukamatwa kwa watu watano wakituhumiwa kulima bangi kwenye mashamba ya ukubwa wa ekari saba katika kijiji cha Ngoma, Kata ya Katete inayopakana na nchi jirani ya Zambia.
Binyura amewaagiza maofisa watendaji wa vijiji na kata zilizopo wilayani humo kuwabaini wanaolima bangi na kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua za haraka zichukuliwe huku akionya kuwa wakishindwa kufanya hivyo, kila mtumishi wa umma aliyeko katika maeneo hayo ya utawala wasaidie kuwafichua wahalifu hao.
Wilayani Nkasi watu wawili wakazi wa kijiji cha Nkundi kilichopo katika Kata ya Kipande wilayani humo wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma ya kulima bangi.
Waliokamatwa wametajwa kuwa ni pamoja na Oscar Msangawale na Thobias Malambo waliokutwa wanalima bangi kwenye mashamba yao na bustani zao kwa pamoja yakiwa na ukubwa wa ekari moja.
Katibu Tawala wa Wilaya Nkasi , Festo Chonya alidai kuwa walipata taarifa za kuwapo kwa shamba la bangi katika kijiji hicho ambapo Kamati ya Ulinzi na Usalama ilifika eneo la tukio na kukuta bangi ikiwa imelimwa katika shamba lenye ukubwa wa zaidi ya ekari moja.
Akifafanua, alisema shamba la bangi lenye ukubwa wa zaidi ya ekari moja linamilikiwa na Msangawale ambapo Malambo yeye alikutwa na bangi ikiwa imeoteshwa kwenye bustani ya maua iliyopo pembeni ya nyumba yake ya kuishi. Kufuatia msako huo, Polisi walifanikiwa kuiteketeza kwa moto bangi yote iliyovunwa katika shamba hilo

MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA

KATIKA kupambana na uhalifu wa dawa za kulevya, Shirika la Posta Tanzania (TPC), linasimika mfumo wa kisasa utakaogharimu Sh. Milioni 200 wa kudhibiti usalama na kurahisisha utambuzi wa vitu na matukio hatarishi na haramu yanayopitishwa au kujitokeza kupitia mtandao wa shirika hilo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo, Dk Haruni Kondo amesema leo alipokuwa akizungumza jijini Dar es Salaam. Dk Kondo alisema mfumo huo unajumuisha ufungaji wa kamera za kiusalama (CCTV), katika Posta Kuu ya Dar es Salaam, na tayari mzabuni aliyeusimika ameshakamilisha kazi yake na ataukabidhi kwa shirika wiki ijayo. Utazinduliwa rasmi wakati wowote kuanzia hapo.
"Aidha tumesimika mifumo ya kisasa ya kiusalama ikiwa ni pamoja na mashine za ukaguzi wa mizigo katika ofisi zenye uwezekano wa kuwa uchochoro wa uhalifu wa aina hii ikiwa ni pamoja na ofisi za Zanzibar, Kigoma, Dar es Salaam na Arusha," amesema.
Amesema hatua hizo zimechukuliwa na shirika ili kuhakikisha linashiriki na kuchangia kikamilifu jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kupambana na uhalifu, ikiwa ni pamoja na usafirishaji, uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya, usafirishaji na utakatishaji wa fedha haramu, ugaidi, udaganyifu katika utambulisho pamoja na uhalifu mwingine wa kimtandao wa kitaifa na kimataifa.
Mwenyekiti huyo alisema Bodi ya Wakurugenzi ya shirika imedhamiria kuongeza msukumo wa kasi ya usimamizi ili kupambana na uhalifu huo ambao una madhara makubwa kwa jamii.
Amesema hatua hiyo imechukuliwa kwa kuzingatia kuwa matukio ya uhalifu uliopangwa yamekuwa ni changamoto kubwa kwa mashirika ya Posta duniani.
Ametaja vitu visivyoruhusiwa kusafirishwa katika mtandao wa Posta kwa mujibu wa sheria kuwa ni pamoja na dawa za kulevya, bidhaa za kemikali zenye sumu, silaha za moto na milipuko, wanyama hai, nyara za serikali, vifaa vya mionzi, vyakula vinavyooza, betri za aina mbalimbali, vimiminika, fedha haramu, utakatishaji wa fedha na vitu vyovyote hatarishi.


Shirika hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usimamizi wa sheria, kwa hivi sasa limeimarisha uhakiki wa mifumo yake na pia ukaguzi wa barua, vifurushi, vipeto na mizigo ili kujiridhisha juu ya usalama na uzingatiaji wa sheria.

ZIARA YA RAIS WA UGANDA YOWERI MUSEVENI

RAIS John Magufuli ameitaka Kampuni ya Total inayowekeza katika ujenzi wa bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 1,443 kutoka Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga, kuacha visingizio na kuanza ujenzi wa bomba hilo mara moja.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati wa ziara ya siku mbili ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais Magufuli alisema serikali imeshughulikia masharti yote saba ambayo mwekezaji hayo aliyataka.
“Masharti aliyoyataka kwa upande wa Tanzania yameshashughulikiwa yote ikiwa ni pamoja na suala la msamaha wa kodi ya thamani. Hivyo hili si tatizo tena, mhusika aambiwe asitafute visingizio vidogovigo vya kushindwa kujenga halafu akasingizia mahali fulani hawafanyi kumbe yeye ni tatizo.
Alisema pia serikali imetoa fursa nyingi kwa mwekezaji huyo ili kurahisisha kazi yake ya ujenzi wa bomba hilo huku akisisitiza kama kuna mambo madogo madogo yanajitokeza yashughilikiwe huku ujenzi ukiendelea.
Rais Magufuli alisema katika kuonesha dhamira ya kweli ya kuhakikisha mradi huo unafanikiwa, Serikali imeshaanza upanuzi wa bandari ya Tanga ili kuwezesha shughuli za ujenzi wa bomba hilo kwenda vizuri.
“Tanzania tuna uzoefu na masuala ya ujenzi wa mabomba, hili litakuwa bomba la tatu kujengwa kwani kuna bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Zambia (TAZAMA) na lile la la gesi asili (kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam),” alisema.
Aliongeza; “Tumeamua tuwakubalie ndugu zetu waganda, kwa sababau waganda ni ndugu zetu, masuala mazuri ya Uganda ni lazima tuyapokee sisi kwa mikono miwili na ndio maana nimemhahakikishia rais kuwa bomba lilitakiwa lianze kujengwa jana kwa sababu sisi hatuna tatizo.”
Rais Magufuli alisema hata maeneo ambayo bomba hilo litapita ambayo ni ya hifadhi ya barabara, Serikali itahakikisha inalitatua hilo ili kuhakikisha bomba hilo linapita na kujengwa.
Rais Museveni baada ya kufanya mazungumzo na Rais Magufuli kuhusu suala la ujenzi wa bomba la mafuta, aliahidi kufuatilia baadhi ya mambo kwa upande wa nchi yake ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kama ulivyopangwa.
“Tumegundua mafuta mwaka 2006 hata kabla ya Ghana, lakini kwa muda mrefu yamebaki ardhini kwa sababu kuna baadhi ya makampuni makubwa yalitaka kufanya udanganyifu wa njia ya kipitisha mafuta.
“Hatimaye sasa tumepata njia ya kupitisha mafuta, hivyo hatuna sababu ya kuendelea kupoteza muda kwa sababu utatupa fedha ambazo zitasaidia kuboresha miundombinu na kuibadili kabisa nchi yetu,” alisema.
Aidha, viongozi hao wawili wamekubaliana mwekezaji huyo kuanza mchakato wa kuhakikisha jiwe la msingi la ujenzi wa bomba hilo haraka iwekezenavyo.


Rais Museveni ameishukuru serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi miwili ya umeme ambayo itasaidia vijiji vilivyoko Tanzania na vile vya Uganda kupata umeme wa uhakika.

SHIZZA KICHUYA TENA

SHIZZA Kichuya jana alikuwa shujaa wa Simba baada ya kuifungia bao la ushindi katika mechi ya Ligi Kuu bara dhidi ya Yanga iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi hiyo ya raundi ya pili na kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 54 juu ya mabingwa watetezi Yanga wenye pointi 49 lakini wakiwa na mchezo kibindoni.
Kichuya aliyeingia uwanjani katika dakika ya 51 kuchukua nafasi ya Novaty Lufunga alifunga bao hilo kwa shuti kali nje ya 18 na kuipa timu yake pointi tatu muhimu katika mbio za ubingwa ambao haujatua mtaa wa Msimbazi kwa kwa karibu mwaka wanne sasa.
Mchezaji huyo anaifunga mara ya pili Yanga msimu huu, mara ya kwanza ilikuwa kwenye mechi ya raundi ya kwanza Oktoba Mosi mwaka jana alipofunga bao la kusawazisha timu hizo zilipotoka sare ya bao 1-1.
Katika mechi ya jana, Simba ililazimika kucheza pungufu karibu kipindi chote cha pili baada ya mwamuzi Mathew Akrama wa Mwanza kumtoa nje kwa kadi nyekundu Besela Bukungu aliyemtendea madhambi Obrey Chirwa aliyekuwa akielekea kufunga bao la pili wakati Yanga ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Yanga ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza katika dakika ya tano ya mchezo huo kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi Akrama baada ya Lufunga kumchezea vibaya kwenye eneo la hatari Chirwa.
Bao hilo liliichanganya Simba ambayo sasa wachezaji wake walionekana kutotulia uwanjani na katika dakika ya 26 benchi la ufundi chini ya kocha wake Mkuu Joseph Omog lilifanya mabadiliko kwa kumtoa Juma Luizio na nafasi yake kuchukuliwa na Said Ndemla.
Dakika tatu baadae Laudit Mavugo anaikosesha Simba bao akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga lakini anapiga mpira pembeni.
Simba ilikuwa na nafasi nyingine ya kupata bao la kusawazisha katika dakika ya 35 baada ya mwamauzi kuwapa mpira wa adhabu nje ya 18 lakini Ndemla alipaisha mpira huo.
Hata hivyo pamoja na kubaki pungufu kuanzia dakika ya 55 kwa kutolewa Bukungu, Simba iliendelea kuimarika na katika dakika ya 66, nyota ya Mrundi Mavugo iliendelea kung’ara baada ya kufunga bao la kusawazisha kwa kichwa akiunganisha mpira wa Shizza Kichuya.
Hiyo ni mechi ya nne mfululizo kwa Mavugo kufunga katika michuano yote kwa Simba tangu alipoanza kucheza dakika 90.
Awali alikuwa akiingia dakika za mwishoni mwa kipindi cha pili na alioenekana hana mchango wa timu mpaka benchi la ufundi lilipoamua kufanya mabadiliko na kumuanzisha kwa dakika zote.
Aidha katika mechi hiyo baada ya Simba kuwa mbele kwa mabao 2-1 baadhi ya mashabiki wa pande zote mbili walizimia kwa nyakati tofauti, mashabiki wa Simba wakizimia kwa furaha na Yanga kwa majonzi. Kabla ya mechi kuanza wachezaji wa timu zote walisimama kwa dakika moja kumkumbuka aliyekuwa mchezaji wa Yanga na Taifa Stars Geofrey Bonny aliyefariki dunia wiki iliyopita.
Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’, Kelvin Yondani, Juma Abdul, Vincent Andrew, Haruna Niyonzima, Amis Tambwe/ Deus Kaseke dk 70, Obrey Chirwa, Thaban Kamusoko/Juma Makapu dk 44, Justine Zullu/ Juma Mahadhi dk 78, Mwinyi Haji, Simon Msuva.


Simba: Daniel Agyei, Abdi Banda, Mohamed Hussein, Besela Bukungu, Novalty Lufunga/ Shizza Kichuya dk 51, James Kotei, Ibrahim Ajib, Laudit Mavugo, Mohamed Ibrahim/Jonas Mkude dk 57, Mzamiru Yassin, Juma Luizio/Said Ndemla dk 26.

Wednesday, 15 February 2017





BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limesitisha mpango wa kuwafanyia mtihani wa udahili wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu katika shule za sekondari za serikali uliokuwa ufanyike Februari 28, mwaka huu.
Naibu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani Salumu alisema hayo juzi kwenye kikao cha wadau wa sekta ya elimu Mkoa wa Morogoro alipokuwa akihitimisha mada yake kwa wajumbe wa kikao hicho kilichoongozwa na mkuu wa mkoa huo, Dk Stephen Kebwe.
Salumu alisema mpango wa kuwafanyia mtihani wa udahili wanafunzi hao ulitokana na matakwa yaliyowasilishwa Necta na baadhi ya wakuu wa shule za serikali wakipendekeza kupitia maofisa elimu wa mikoa na wilaya kuwa wanafunzi wa kidato cha kwanza waliochaguliwa na kupangiwa shule zao wengi hawana sifa na uwezo wa kumudu masomo.
Naibu Katibu Mtendaji wa Necta alisema wakuu wa shule walikuwa wakiomba kupata idhini ya kuwafanyia mtihani wanafunzi ili kubaini uwezo wao na kwamba baraza liliwasiliana na maofisa elimu mkoa na wilaya likiwataka kuwasilisha orodha ya idadi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza waliopangiwa kwenye shule ya zao.
Alisema baada ya kufahamika idadi ya wanafunzi hao, baraza ndilo litatunga maswali ya mitihani yenye kuzingatia mfumo na vigezo maalumu na kutumiwa wakuu wa shule hizo ili kuusimamia kwa lengo la kuweka uzani sawa wa mtihani huo.
Alisema moja ya masharti ni kwamba mtihani huo ulitakiwa ufanyike kwa wanafunzi wa kidato hicho kwa shule zote za serikali siku moja na kwa muda uliopangwa.
Hata hivyo, alisema baada ya kuwatumia masharti hayo, wakuu wa shule hizo walishindwa kuwasilisha orodha ya wanafunzi kwa maofisa elimu wa mikoa na wilaya ili itumwe Necta na kutokana na mazingira hayo, baraza limeamua kusitisha kuwadahili wanafunzi wa kidato cha kwanza na kuitaka mamlaka inayosimamia elimu kuendelea na utaratibu wao wa kawaida.
“Necta imewasiliana na wahusika kwa barua rasmi ya kusitisha mtihani huo ambao ulipangwa ufanyike Februari 28, mwaka huu na wanafunzi wote waliopangiwa kidato cha kwanza shule mbalimbali za serikali zikiwemo za bweni, waendelee na masomo kama yalivyopangwa,” alieleza Naibu Katibu Mtendaji wa Necta.
Novemba mwaka jana, serikali ilitangaza kuwa wanafunzi 526,653 sawa na asilimia 94.8 ya waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana, wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari za serikali katika awamu ya kwanza huku 28,638 wakishindwa kupangiwa shule katika awamu ya kwanza.
Kati ya wanafunzi hao, wasichana ni 268,052 sawa na asilimia 94.5 ya wasichana waliofaulu na wavulana ni 258,601 sawa na asilimia 95.2 ya wavulana waliofaulu.

Ma-RPC waongeza nguvu vita ya ‘unga’

SASA ni dhahiri kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya si suala la mzaha na litagusa kila kona ya Tanzania na kutomwacha mshukiwa yeyote.
Katika kuhakikisha kuwa biashara hiyo haramu inakomeshwa nchini na kwa kuzingatia dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kupambana na tatizo hilo, Jeshi la Polisi limetoa maelekezo kwa makamanda wa Polisi katika mikoa yote, kuongeza nguvu za oparesheni katika mapambano kwa kuwakamata wanaotumia, wanaouza na wanaosafirisha.
Polisi imewaagiza makamanda wote pindi wanapoendesha oparesheni dhidi ya dawa za kulevya, kutokuangalia sura ya mtu, cheo, wadhifa wala nafasi aliyonayo katika jamii.
Hayo yamebainishwa katika taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa jana na Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Bulimba kwa vyombo vya habari.
“Katika kuhakikisha kuwa biashara haramu ya dawa za kulevya inakomeshwa hapa nchini na kwa kuzingatia dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kupambana na tatizo la dawa za kulevya, Jeshi la Polisi nchini limetoa maelekezo kwa makamanda wa Polisi katika mikoa yote kuongeza nguvu za oparesheni katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya kwa kuwakamata wanaotumia, wanaouza na wanaosafirisha,” ilieleza taarifa ya Bulimba.
Kwa nyakati tofauti tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipotangaza vita dhidi ya dawa za kulevya na kutaja hadharani majina ya watu wanaohusishwa na dawa hizo kwa kutumia, kuuza au kusafirisha, Rais John Magufuli aliweka bayana kwamba hiyo siyo vita ya Makonda pekee yake.
Rais Magufuli pamoja na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Rogers Sianga wameeleza kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya ni ya Watanzania wote, na kwamba haitajali sura ya mtu, wadhifa, rangi, kabila wala cheo chake, bali itamkumba yeyote anayejihusisha nayo.
“Tuta deal (shughulika) na mtu yeyote, wale ambao wanadhani sheria hii ambayo inaipa mamlaka serikali kusimamia vita ya dawa za kulevya haifai, wapeleke bungeni ikafanyiwe marekebisho hasa Kifungu cha 10,” alisema Dk Magufuli wakati akimwapisha Sianga, Ikulu mwishoni mwa wiki.
Alisema serikali itaisimamia sheria hiyo Namba 5 ya mwaka 2015, na hawatajali mtu yeyote, awe mbunge, mwanasiasa, waziri, mchungaji, padri au shehe.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi nchini limekemea tabia ya baadhi ya wananchi wanaokusanyika katika vituo vya Polisi pindi baadhi ya watuhumiwa wa makosa mbalimbali wanapotakiwa kufika kwenye vituo hivyo kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu tuhuma wanazokabiliwa nazo.
“Ni marufuku kwa mtu ama kikundi chochote kukusanyika katika kituo cha Polisi bila ya kuwa na sababu ya msingi na watakaobainika watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria,” alieleza Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Alitoa mwito kwa kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, zikiwemo za watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na taarifa hizo zitafanyiwa kazi kwa siri ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa katika hali ya usalama.
Wakati Jeshi la Polisi likiagiza hayo, tayari Polisi mkoani Arusha limekamatwa watuhumiwa wa dawa za kulevya, bangi na mirungi akiwemo askari aliyejihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu.
Miongoni mwa madawa yaliyokamatwa jijini Arusha kwenye msako uliofanyika Februari 7, mwaka huu kwenye viunga mbalimbali vya Jiji la Arusha ni mirungi yenye kilogramu 33, kete 167 za dawa ya kulevya aina ya heroin na bangi misokoto 3,845.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Charles Mkumbo alisema watuhumiwa 54 walikamatwa kutokana na kukutwa na misokoto 3,845 ya bangi huku waliokamatwa na mirungi yenye kilogramu 33 wakiwa 12 pamoja na 14 waliokamatwa wakiwa na kete 167 za heroin.
Alisema miongoni mwa watuhimwa hao waliokamatwa na bangi, kuna wauzaji wa madawa hayo ambao idadi yao ni 40, msafirishaji mmoja na wanaojihusisha ni 14 na askari mmoja mwenye namba za kijeshi F.6978 D/CPL Zakayo, ambaye naye anashikiliwa huku uchunguzi dhidi yake ukiendelea kufanyika.
“Bado tunaendelea na misako maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha na sasa hivi atakayekamtwa atafikishwa kwenye vyombo vya dola na polisi huyo tunamshikilia kwa sababu amekuwa ni mtovu wa nidhamu, lakini pia anawabambikizia watu kesi kwa kuwashikiza bangi ili apewe fedha,” alieleza Kamanda Mkumbo.