Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi hiyo ya raundi ya pili na kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 54 juu ya mabingwa watetezi Yanga wenye pointi 49 lakini wakiwa na mchezo kibindoni.
Kichuya aliyeingia uwanjani katika dakika ya 51 kuchukua nafasi ya Novaty Lufunga alifunga bao hilo kwa shuti kali nje ya 18 na kuipa timu yake pointi tatu muhimu katika mbio za ubingwa ambao haujatua mtaa wa Msimbazi kwa kwa karibu mwaka wanne sasa.
Mchezaji huyo anaifunga mara ya pili Yanga msimu huu, mara ya kwanza ilikuwa kwenye mechi ya raundi ya kwanza Oktoba Mosi mwaka jana alipofunga bao la kusawazisha timu hizo zilipotoka sare ya bao 1-1.
Katika mechi ya jana, Simba ililazimika kucheza pungufu karibu kipindi chote cha pili baada ya mwamuzi Mathew Akrama wa Mwanza kumtoa nje kwa kadi nyekundu Besela Bukungu aliyemtendea madhambi Obrey Chirwa aliyekuwa akielekea kufunga bao la pili wakati Yanga ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Yanga ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza katika dakika ya tano ya mchezo huo kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi Akrama baada ya Lufunga kumchezea vibaya kwenye eneo la hatari Chirwa.
Bao hilo liliichanganya Simba ambayo sasa wachezaji wake walionekana kutotulia uwanjani na katika dakika ya 26 benchi la ufundi chini ya kocha wake Mkuu Joseph Omog lilifanya mabadiliko kwa kumtoa Juma Luizio na nafasi yake kuchukuliwa na Said Ndemla.
Dakika tatu baadae Laudit Mavugo anaikosesha Simba bao akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga lakini anapiga mpira pembeni.
Simba ilikuwa na nafasi nyingine ya kupata bao la kusawazisha katika dakika ya 35 baada ya mwamauzi kuwapa mpira wa adhabu nje ya 18 lakini Ndemla alipaisha mpira huo.
Hata hivyo pamoja na kubaki pungufu kuanzia dakika ya 55 kwa kutolewa Bukungu, Simba iliendelea kuimarika na katika dakika ya 66, nyota ya Mrundi Mavugo iliendelea kung’ara baada ya kufunga bao la kusawazisha kwa kichwa akiunganisha mpira wa Shizza Kichuya.
Hiyo ni mechi ya nne mfululizo kwa Mavugo kufunga katika michuano yote kwa Simba tangu alipoanza kucheza dakika 90.
Awali alikuwa akiingia dakika za mwishoni mwa kipindi cha pili na alioenekana hana mchango wa timu mpaka benchi la ufundi lilipoamua kufanya mabadiliko na kumuanzisha kwa dakika zote.
Aidha katika mechi hiyo baada ya Simba kuwa mbele kwa mabao 2-1 baadhi ya mashabiki wa pande zote mbili walizimia kwa nyakati tofauti, mashabiki wa Simba wakizimia kwa furaha na Yanga kwa majonzi. Kabla ya mechi kuanza wachezaji wa timu zote walisimama kwa dakika moja kumkumbuka aliyekuwa mchezaji wa Yanga na Taifa Stars Geofrey Bonny aliyefariki dunia wiki iliyopita.
Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’, Kelvin Yondani, Juma Abdul, Vincent Andrew, Haruna Niyonzima, Amis Tambwe/ Deus Kaseke dk 70, Obrey Chirwa, Thaban Kamusoko/Juma Makapu dk 44, Justine Zullu/ Juma Mahadhi dk 78, Mwinyi Haji, Simon Msuva.
Simba: Daniel Agyei, Abdi Banda, Mohamed Hussein, Besela Bukungu, Novalty Lufunga/ Shizza Kichuya dk 51, James Kotei, Ibrahim Ajib, Laudit Mavugo, Mohamed Ibrahim/Jonas Mkude dk 57, Mzamiru Yassin, Juma Luizio/Said Ndemla dk 26.
No comments:
Post a Comment
Phone: +255745767927
Email: jeremiahelijah01@gmail.com
facebook page: OMBLOX