Monday, 30 January 2017

WATU kadhaa wamejeruhiwa

WATU kadhaa wamejeruhiwa, mmoja akiwa ana hali mbaya baada ya mabehewa tisa ya treni ya abiria ya Deluxe, iliyokuwa ikitoka mkoani Kigoma kwenda Dar es Salaam kuanguka mkoani Pwani.
Katika mabehewa hayo, manne yameanguka, matatu yameacha njia na mawili yametenguka.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Boniventure Mushongi, mabehewa yaliyoanguka ni saba na kwamba wanaendelea kuwaokoa majeruhi.
Akizungumza kwa njia ya simu, Msemaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Midladjy Maez alisema ajali hiyo ilitokea saa 9:40 alasiri katika Kitongoji cha Kambini Ruvu Ngeta, Kata ya Kikongoa Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani. Maez alisema mabehewa hayo yalianguka baada ya treni kuacha njia na kusababisha majeruhi kadhaa.
“Ni kweli ajali hiyo imetokea na kusababisha majeruhi na hadi wakati huo kulikuwa hakuna taarifa yoyote ya kifo kilichotokana na ajali hiyo, licha ya kwamba mtu mmoja ndiyo hali yake mbaya,” alisema Maez, bila kutaja sababu za ajali hiyo.
“...Imeripotiwa watu kadhaa wamejeruhiwa na mmoja amejeruhiwa sana, hizi ni taarifa za awali…baada ya kikosi cha uokoaji kumaliza kazi ya kuinua mabehewa ndio taarifa ya waathirika itakamilika,” alisema Maez katika taarifa yake.
Alisema treni hiyo ilitakiwa ifike Dar es Salaam saa 11 jioni, lakini ilipofika hapo mabehewa hayo yalianguka na kusababisha kushindwa kuendelea na safari.
“Kutokana na ajili hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Mkurugenzi Mkuu wa TRL wanaelekea eneo la tukio ili kuweza kujua kilichotokea,” aliongeza msemaji huyo wa TRL.

Friday, 27 January 2017

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas

SIMBA sasa iko salama kuendelea na michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) baada ya TFF kuitupilia mbali rufaa ya klabu ya Polisi Dar es Salaam iliyokuwa ikitaka Simba ipokwe ushindi kwa kumchezesha mchezaji Novatus Lufunga katika mchezo wao wa raundi ya tano ya michuano hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Lufunga alioneshwa kadi nyekundu katika mechi ya robo fainali ya michuano hiyo msimu uliopita dhidi ya Coastal Union kwa kumchezea vibaya Ally Shiboli, hivyo kwa mujibu wa kanuni za michuano hiyo alipaswa kutumikia adhabu hiyo kwa kukosa mechi iliyopita.
Mechi hiyo ya mwishoni mwa wiki iliyopita iliyochezwa kwenye uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, Simba ilishinda kwa mabao 2-0 na kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema jana kuwa rufaa hiyo ilichelewa kufika kwao na haikuwa na ada na hivyo imetupwa kwa mujibu wa kanuni ya 18 (1) na (2) ya Kanuni za Kombe la Shirikisho la Azam.
Kanuni ya 18 (1) inasema: “Malalamiko yoyote kuhusu mchezo yawasilishwe kwa maandishi kwa kamishna wa mchezo au TFF sio zaidi ya saa 72 baada ya kumalizika mchezo”.
Kwa mujibu wa Lucas, kanuni ya 18 (2) inasema: Ada ya malalamiko ni Sh 300,000 na malalamiko yoyote yatakayowasilishwa bila kulipiwa ada na kuwasilishwa nje ya muda uliowekwa hayatasikilizwa.
Alitolea ufafanuzi kuhusu kadi nyekundu aliyopewa Lufunga msimu uliopita, alisema kwa utaratibu wa mashindano hayo ambayo ni ya mtoano, adhabu za kadi (njano na nyekundu) zitolewazo uwanjani, zinakoma mwisho wa msimu wa shindano husika isipokuwa kadi hizo zikiongezwa adhabu ya kinidhamu ambayo itafahamishwa kwa klabu na mchezaji kwa maandishi.
Pia, alisema kanuni ya 16 ya Kombe la Shirikisho Sehemu ya Tatu inaeleza wazi kuwa matumizi ya kanuni za ligi zitahusika maeneo yanayoruhusu uendeshaji wa shindano la mtoano.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga



WATU 14 akiwemo Mchina, wanahofiwa kufa baada ya kufukiwa katika mgodi wa dhahabu wa Kampuni ya RZ Union Mining Ltd uliopo Kata ya Nyarugusu mkoani Geita.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga alisema watu hao wamefukiwa chini ya mgodi baada ya mlango wa kuingilia kwenye shimo la mgodi kumeguka udongo na kujiziba.
“Usiku wa kuamkia leo (jana) saa tisa kwenye mgodi huo unaoendeshwa na Wachina, mlango wa kuingilia mgodini mmoja ulimeguka na kujifunga watu 14 wakiwa ndani,” alisema Kyunga.
Kyunga alisema kwa mujibu wa kitabu cha orodha ya watu wanaojiandikisha kuingia mgodini, kuna majina ya Watanzania 12 na Mchina.
Aidha, alisema mbali na watu hao 13, pia kuna Mtanzania mmoja ambaye aliingia bila kujiandikisha na hiyo ni kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo hivyo kufanya idadi ya watu waliofukiwa kuwa 14. Kyunga alisema tangu jana asubuhi jitihada mbalimbali za kuondoa udongo kuwaokoa watu hao zinaendelea wakitumia mitambo na wataalamu.
“Kwa kusaidiana na Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) na wataalamu wengine, jitihada zinaendelea ili kuhakikisha tunawaokoa watu hao,” alisema Kyunga. Alisema wakati huo huo wamefanikiwa kutoboa eneo jingine na kupitisha mabomba ya hewa ya oksijeni ili kuwafanya watu hao wasikose hewa.

SAFARI YA DODOMA


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto , Ummy Mwalimu .
  


WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto itahamia Dodoma ndani ya siku 14 zijazo.
Waziri Ummy Mwalimu amesema tayari wizara yake imejiandaa kuhamia Dodoma, kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la serikali kuhamia Dodoma kabla ya 2020.
“Tutahamia Dodoma ndani ya muda wa wiki mbili,” alisema Ummy wakati akifungua semina ya kitaifa ya afya mjini hapa juzi. Aliwatangazia wadau wa afya nchini kwamba atatangaza kabla ya kuhamia Dodoma ni huduma gani zitaendelea kutolewa Dar es Salaam na zile zitakazohamishiwa Dodoma.
Alithibitisha kwamba ofisi yake kama waziri, ya naibu waziri, na Katibu Mkuu wake wa wizara, hazitabaki Dar es Salaam, bali zitakuwa Dodoma.
Kuhamia kwa wizara hiyo Dodoma, itakuwa ni wizara ya tano, uhamisho huyo ulitanguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyehamia Septemba mwaka jana na baadaye akafuata Waziri wa Nchi katika ofisi yake, Jenista Mhagama anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu.
Mawaziri wengine waliohamia Dodoma ni wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene na msaidizi wake, Selemani Jafo pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki.
Kutokana na ratiba iliyotangazwa na Waziri Mkuu mwaka jana, waziri mkuu na mawaziri wote pamoja na makatibu wakuu wa wizara, wanatakiwa kuwa tayari wamehamia Dodoma kufikia Februari 28, mwaka huu.
Ratiba hiyo inaonesha kati ya Machi na Agosti mwaka huu, watendaji wa wizara wanatakiwa kupanga na kutenga bajeti kwa maofisa wao kuhamia makao makuu ya nchi.

TRA YAWAKUMBUKA WALEMAVU MWANZA

TRA YAWAKUMBUKA WALEMAVU MWANZA.


Kwa mara ya kwanza mamlaka ya mapato Tanzania(TRA)mkoa wa Mwanza imewakumbuka wajasiriamali wenye ulemavu wa kutosikia (viziwi) na kutoongea (mabubu) kwa kuwaelimisha masuala ya ujasiriamali,kodi na mbinu za biashara.

Akitoa mada ya ujasiriamali na kodi,ofisa mwandamizi wa huduma na elimu ya kodi wa TRA mkoa wa Mwanza Lutufyo Mtafya, alitaja sifa za mjasiriamalikua ni uwezo,ubunifu,kujiamini,kujituma,kuona fursa na kukabili vikwazo.

Akisisitiza Mtafya alisema wafanya biashara wanapokosa vibali ni wazi kwamba  hawezi kupata zabuni kubwa,bila kusita kuwatumia watu wenye uzoefu,vipaji na mtaji.

 Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Mkoa wa Mwanza, Jones George na mkalimani kutoka Chama cha Wakalimani wa Lugha ya Alama Tanzania, Subira Joseph, aliupongeza uongozi wa TRA mkoani hapa kutokana na hatua hiyo ya kuwakumbuka walemavu hao katika elimu ya ujasiriamali na kodi.