Friday, 27 January 2017

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas

SIMBA sasa iko salama kuendelea na michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) baada ya TFF kuitupilia mbali rufaa ya klabu ya Polisi Dar es Salaam iliyokuwa ikitaka Simba ipokwe ushindi kwa kumchezesha mchezaji Novatus Lufunga katika mchezo wao wa raundi ya tano ya michuano hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Lufunga alioneshwa kadi nyekundu katika mechi ya robo fainali ya michuano hiyo msimu uliopita dhidi ya Coastal Union kwa kumchezea vibaya Ally Shiboli, hivyo kwa mujibu wa kanuni za michuano hiyo alipaswa kutumikia adhabu hiyo kwa kukosa mechi iliyopita.
Mechi hiyo ya mwishoni mwa wiki iliyopita iliyochezwa kwenye uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, Simba ilishinda kwa mabao 2-0 na kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema jana kuwa rufaa hiyo ilichelewa kufika kwao na haikuwa na ada na hivyo imetupwa kwa mujibu wa kanuni ya 18 (1) na (2) ya Kanuni za Kombe la Shirikisho la Azam.
Kanuni ya 18 (1) inasema: “Malalamiko yoyote kuhusu mchezo yawasilishwe kwa maandishi kwa kamishna wa mchezo au TFF sio zaidi ya saa 72 baada ya kumalizika mchezo”.
Kwa mujibu wa Lucas, kanuni ya 18 (2) inasema: Ada ya malalamiko ni Sh 300,000 na malalamiko yoyote yatakayowasilishwa bila kulipiwa ada na kuwasilishwa nje ya muda uliowekwa hayatasikilizwa.
Alitolea ufafanuzi kuhusu kadi nyekundu aliyopewa Lufunga msimu uliopita, alisema kwa utaratibu wa mashindano hayo ambayo ni ya mtoano, adhabu za kadi (njano na nyekundu) zitolewazo uwanjani, zinakoma mwisho wa msimu wa shindano husika isipokuwa kadi hizo zikiongezwa adhabu ya kinidhamu ambayo itafahamishwa kwa klabu na mchezaji kwa maandishi.
Pia, alisema kanuni ya 16 ya Kombe la Shirikisho Sehemu ya Tatu inaeleza wazi kuwa matumizi ya kanuni za ligi zitahusika maeneo yanayoruhusu uendeshaji wa shindano la mtoano.

No comments:

Post a Comment

Phone: +255745767927
Email: jeremiahelijah01@gmail.com
facebook page: OMBLOX