SASA ni dhahiri kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya si suala la mzaha
na litagusa kila kona ya Tanzania na kutomwacha mshukiwa yeyote.
Katika kuhakikisha kuwa biashara hiyo haramu inakomeshwa nchini na
kwa kuzingatia dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kupambana na
tatizo hilo, Jeshi la Polisi limetoa maelekezo kwa makamanda wa Polisi
katika mikoa yote, kuongeza nguvu za oparesheni katika mapambano kwa
kuwakamata wanaotumia, wanaouza na wanaosafirisha.
Polisi imewaagiza makamanda wote pindi wanapoendesha oparesheni dhidi
ya dawa za kulevya, kutokuangalia sura ya mtu, cheo, wadhifa wala
nafasi aliyonayo katika jamii.
Hayo yamebainishwa katika taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa jana
na Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Bulimba kwa vyombo vya habari.
“Katika kuhakikisha kuwa biashara haramu ya dawa za kulevya
inakomeshwa hapa nchini na kwa kuzingatia dhamira ya Serikali ya Awamu
ya Tano ya kupambana na tatizo la dawa za kulevya, Jeshi la Polisi
nchini limetoa maelekezo kwa makamanda wa Polisi katika mikoa yote
kuongeza nguvu za oparesheni katika mapambano dhidi ya biashara haramu
ya dawa za kulevya kwa kuwakamata wanaotumia, wanaouza na
wanaosafirisha,” ilieleza taarifa ya Bulimba.
Kwa nyakati tofauti tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
alipotangaza vita dhidi ya dawa za kulevya na kutaja hadharani majina
ya watu wanaohusishwa na dawa hizo kwa kutumia, kuuza au kusafirisha,
Rais John Magufuli aliweka bayana kwamba hiyo siyo vita ya Makonda pekee
yake.
Rais Magufuli pamoja na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za
Kulevya, Rogers Sianga wameeleza kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya ni
ya Watanzania wote, na kwamba haitajali sura ya mtu, wadhifa, rangi,
kabila wala cheo chake, bali itamkumba yeyote anayejihusisha nayo.
“Tuta deal (shughulika) na mtu yeyote, wale ambao wanadhani sheria
hii ambayo inaipa mamlaka serikali kusimamia vita ya dawa za kulevya
haifai, wapeleke bungeni ikafanyiwe marekebisho hasa Kifungu cha 10,”
alisema Dk Magufuli wakati akimwapisha Sianga, Ikulu mwishoni mwa wiki.
Alisema serikali itaisimamia sheria hiyo Namba 5 ya mwaka 2015, na
hawatajali mtu yeyote, awe mbunge, mwanasiasa, waziri, mchungaji, padri
au shehe.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi nchini limekemea tabia ya
baadhi ya wananchi wanaokusanyika katika vituo vya Polisi pindi baadhi
ya watuhumiwa wa makosa mbalimbali wanapotakiwa kufika kwenye vituo
hivyo kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu tuhuma wanazokabiliwa nazo.
“Ni marufuku kwa mtu ama kikundi chochote kukusanyika katika kituo
cha Polisi bila ya kuwa na sababu ya msingi na watakaobainika
watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria,” alieleza Msemaji wa Jeshi la
Polisi.
Alitoa mwito kwa kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na
wahalifu, zikiwemo za watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za
kulevya na taarifa hizo zitafanyiwa kazi kwa siri ili kuhakikisha nchi
inaendelea kuwa katika hali ya usalama.
Wakati Jeshi la Polisi likiagiza hayo, tayari Polisi mkoani Arusha
limekamatwa watuhumiwa wa dawa za kulevya, bangi na mirungi akiwemo
askari aliyejihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu.
Miongoni mwa madawa yaliyokamatwa jijini Arusha kwenye msako
uliofanyika Februari 7, mwaka huu kwenye viunga mbalimbali vya Jiji la
Arusha ni mirungi yenye kilogramu 33, kete 167 za dawa ya kulevya aina
ya heroin na bangi misokoto 3,845.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa
Mkoa, Charles Mkumbo alisema watuhumiwa 54 walikamatwa kutokana na
kukutwa na misokoto 3,845 ya bangi huku waliokamatwa na mirungi yenye
kilogramu 33 wakiwa 12 pamoja na 14 waliokamatwa wakiwa na kete 167 za
heroin.
Alisema miongoni mwa watuhimwa hao waliokamatwa na bangi, kuna
wauzaji wa madawa hayo ambao idadi yao ni 40, msafirishaji mmoja na
wanaojihusisha ni 14 na askari mmoja mwenye namba za kijeshi F.6978
D/CPL Zakayo, ambaye naye anashikiliwa huku uchunguzi dhidi yake
ukiendelea kufanyika.
“Bado tunaendelea na misako maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha na
sasa hivi atakayekamtwa atafikishwa kwenye vyombo vya dola na polisi
huyo tunamshikilia kwa sababu amekuwa ni mtovu wa nidhamu, lakini pia
anawabambikizia watu kesi kwa kuwashikiza bangi ili apewe fedha,”
alieleza Kamanda Mkumbo.